Thursday, December 31, 2009

Pacquiao na Myweather kuchapana mahakamani sasa


Mwanasheria wa bingwa wa dunia uzito wa kati anayeshikilia mkanda wa WBO na IBO Mann Pacquiao, Daniel Patroceli amesema anataka kumfikisha mahakamani bondia Floyd Myweather Jr kutokana na bondia huyo pamoja na kambi yake kwa kumshutmu waziwazi bondia wake kuwa anatumia madawa ya kuongeza nguvu na ndio maana alifanikiwa kuwatwanga mabondia wengine kama Oscar De Lahoya na Richard Schaffer.

Mwanasheria huyo amesema kamwe hawezi kuruhusu na kuona bondia wake akirushiwa shutuma hizo.

Bingwa huyo wa dunia amekataa kuchukua vipimo vya mkojo kabla ya mchezo wake na Myweather Jr na yeye mwenyewe anataka kuchukua vipimo hivyo mara baada tu ya mchezo huo ambao umepangwa kuchezwa tarehe kumi na tatu ya mwezi wa tatu

Liver yapata pigo


Jogoo la Anfield Liverpool wamepata pigo kubwa baada madakari kuthibitisha kuwa mlinzi wake mahiri wa kulia Glen Johnson atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha mwezi mzima hali itakayomfanya kocha mkuu wa miamba hiyo ya Merseyside Rafael Benitez kutafuta mbadala wake.

Liverpool ambao imekuwa haina matokeo mazuri msimu huu, inapigana kufa na kupona kuhakikisha inarudi katika nafasi nne za juu katika ligi kuu ya Uingereza.

Matumla na Marwa kuzichapa kesho


Mabondia wakongwe nchini wa uzito wa Crusier Joseph Marwa "Smart Boy"na Rashid Matumla "Snake Boy" wanatarajia kuzichapa katika pambano lisilo la ubingwa hapo kesho katika sikukuu ya mwaka mpya katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Katika zoezi la kupima uzito, matumla alikutwa na kilo 86 huku Marwa ambaye hivi sasa shughuli zake za kikazi anazifanyia Zanzibar alikuwa na kilo 87.

Tayari mabondia wote wameshatoa tambo huku kila mmoja akijipigia chapuo kumtwanga mwenzake hapo kesho.

Mpambano huo pia unatarajia kuvuta hisia za mashabiki wa Yanga na Simba kama walivyo mabondia hao ambapo Matumla ni mnazi mkubwa wa Simba huku Marwa akiwa ni mnazi wa Yanga.


Wednesday, December 30, 2009

Man, Arsenal zaikimbiza Chelsea




Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Uingereza, Manchester United wameichabanga Wigan kwa goli tano kwa buyu katika dimba la Old Trafford magoli yakiwa wekwa kimiani na Wayne Roney, Michael Carrick, Rafael Da Silva, Dimtar Berbatov na Antonio Valenci.

Nayo Arsenal katika dimba la ugenini imefanikiwa kuichabanga Portsmouth goli nne kwa moja magoli yakifungwa na Eduardo da Silva, Samir Nasri, Aron Ramsey pamoja na kiungo wa Cameroun Alex Song.

Tuesday, December 29, 2009




Wanaspotidesk wakiwa na kifimbo kazi

Man U na Arsenal zafukuzana usiku wa leo




Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Uingereza Manchester United pamoja na washika mtutu wa London, Arsenal wanatarajia kufukuzana vikali katika mfululizo wa mechi za ligi kuu ya Uingereza inayotarajia kuendelea hii leo kwa michezo hiyo.

Wakati Man united ikiwa inaikaribisha timu isiyotabirika ya Wigan katika uwanja wa Old Traffrd huku ikiwa na rekodi ya kushinda michezo saba kati ya tisa iliyocheza katika uwanja huo huku ikiwa imeshwahi kwenda sare na Sunderland na kuchapwa na Aston Villa, wapinzani wao ambao wanafukuzana nao katika mbio za ubngwa Asenal wenyewe watakuwa katika dimba la Fratton Park kucheza na Portsmouth ambayo katika michezo yake minne ya mwisho katika dimba hilo imeshinda mitatu.

Wakati wababe hao wakichuana kuwania ubingwa, Aston Villa wamechabangwa hapo jana na Liverpool kwa goli moja kwa bila na kufifia matumaini ya klabu hiyo kuweza kuchukua ubingwa ama kushika nafasi ya nne za juu lakini kwa ushindi huo umempa ahueni kocha mkuu wa liverpool Rafael Benitez ambaye alionekana kukaribia kukalia kuti kavu.

Kifimbo cha Malkia hichooo! chaelekea Kampala




Kifimbo cha malkia wa Uingereza kinachobeba ujumbe kwa nchi wanachama wa jumuiya ya madola kimeondoka katika jiji la Dar es Salaam na kuelekea katika jiji la Kampala nchini Uganda tayari kwa kufikisha ujumbe wa malkia katika jiji hilo na miji mingine nchini humo kabla ya kuanza kwa michezo ya jumuiya ya madola mwezi wa kumi mwakani.
Mapema katika hafla ya kukipokea kifimbo hicho, Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewataka wanamichezo wa hapa nchini kuanza mazoezi na maandalizi mapema ili waweze kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa huku akilitaka jeshi kurudisha hamasa katika michezo kama zamani ambapo liliweza kutoa wanamichezo mahiri kama Filbert Bayi aliyevunja rekodi ya riadha mbio za mita 1500 katika michezo ya jumuiya ya madola mwaka 1974.




Moro yaanza mazoezi


Klabu ya Moro United inayoshiriki ligi kuu ya Tanzania Bara imeanza mazoezi makali ya kujiwinda na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara ikiwa chini ya kocha mkuu wa klabu hiyo Juma Mwambusi pamoja na katibu mkuu wa klabu hiyo Abeid Mziba.


Akiongea na Blog hii wakati wa mazoezi ya klabu hiyo katika uwanja wa chuo cha Ustawi wa Jamii. Mwambusi amesema timu yake hivi sasa inafanya mazoezi makali ili kufanya vizuri katika mzunguko wa pili huku akiamini kuwa mzunguko huo utakuwa mgumu kuliko wa kwanza kutokana na kila timu kujiandaa vya kutosha.


Moro ambayo haikuwa na matokeo mazuri katika mzunguko wa kwanza wa ligi na kumaliza mzunguko huo ikiwa nafasi ya tisa huku ikishinda michezo mitatu tu inakazi ya ziada ya kuhakikisha inafanya vizuri ili kubakia katika ligi ama kupata nafasi ya kucheza katika michuano ya kimataifa.

Sunday, December 27, 2009

YANGA YAMCHINJA PAKA NA KUBEBA TUSKER







Klabu ya Yanga ya jijni Dar es Salaam wamefanikiwa kubeba ubingwa wa Tusker baada ya kuichabanga timu ngumu ya Sofapaka kutoka nchini Kenya kwa jumla ya goli mbili kwa moja katika mchezo uliochezwa katika dimba la uhuru almaarufu kama "shamba la bibi"

Sofapaka ndio waliokuwa wakwanza kupata goli la kuongoza mara baada ya mlinzi wake wa kulia Wanyama Thomas kukwamisha mpira wavuni kwa mpira wa adhabu ambao ulimshinda mlinda mlango wa Yanga Obren Cirkovic.

Hadi mapumziko Yanga ambayo ilitawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa ilienda mapumziko ikiwa nyuma kwa goli mmoja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi lakini safu ya Yanga ilikuwa butu kukwamisha mpira wavuni na ndipo kocha mkuu wa wanajangwani hao Kostadin Papic aliamua kumpumzisha Jery Tegete na kumuingiza Boniface Ambani na kumtoa pia Shadarack nsajingwa na kumuingiza fred mbuna mabadiliko hayo yalileta uhai kwa Yanga na kufanikiwa kupachika magoli mawili ya haraka haraka kupitia kwa Boniface Ambani na Mrisho Ngasa ndani ya dakika sita za mwisho.

Mara baada ya mchezo huo, Papic mewaambia mashabiki wa Yanga mambo bado kwani kuna mengi mazuri yanakuja huku Robert Matano kocha mkuu wa Sofapaka akimlaumu mwamuzi kwa kuibeba Yanga.
Yanga imetwaa kombe hilo pamoja na shillingi millioni arobaini, huku Sofapaka wakichukua millioni thelathini na simba ambao ndio washindi watatu wakichukua millioni ishirini.

Phiri apata ahueni na ushindi wa tatu


Kocha mkuu wa klabu ya Simba, Patrick Phiri amepata ahueni baada ya timu yake kufanikiwa kuicharaza Tusker ya Kenya goli mbili kwa moja na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu na kuzoa kitita cha shllingi milioni ishirini na tatu.

Phiri ambaye anaaminika ni mmoja ya makocha bora kusini mwa Afrika alishaanza kupata wasiwasi na uwezo wa kikosi chake katika michuano hii ya Tusker hususa uwezo uliooneshwa na timu hiyo katika mchezo wa Simba na Yanga.

Hivi sasa kocha huyo raia wa Zambia anahaha kuhakikisha anarudisha morali wa wachezaji wake kabla ya kuanza kwa duru la pili la ligi kuu ya Tanzania Bara pamoja na kombe la shiikisho ambapo Simba itaanza katika mzunguko wa pili.

WENGER AJIULIZA KWA VILLA



Arsenal mchana wa leo inaikaribisha klabu ya Aston Villa katika mchezo wa ligi kuu ya Uingereza mchezo ambao unatarajia kuwa wa vute ni kuvute kutokana na Aston Villa kuzibana mbavu vigogo vingine vya soka nchini humo kama Manchester Uited, Liverpool na Chelsea.

Tayari kocha mkuu wa klabu hiyo, Arsen Wenger amekaririwa akisema kuwa mchezo huo utakua mgumu kutokana na msimamo wa ligi kuwa wazi hivi sasa kwa timu nne za kwanza kubeba ubingwa huo unaoshkiliwa na Manchester United.


Hadi hivi sasa Villa inarekodi ya kushinda michezo minne mfululizo ya ligi kuu ya uingereza na ni klabu pekee ambayo haijawahi kufungwa katika dimba la Emrates

Thursday, December 24, 2009

Ni Yanga ni Yanga Christmas hiiiii!


Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga wamefanikiwa kuicharaza Simba goli mbili kwa moja katika mchezo uliokuwa wa vuta ni kuvute kwa pande zote mbili katika dimba la uhuru.


Mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Dennis Batte kutoka nchini Uganda ulitawaliwa na ubabe wa kila aina kutoka pande zote mbili hali iliyosababsha mshabuliaji wa Simba Haruna Moshi Boban kuoneshwa kadi nyekundu baada ya kutoa lugha chafu kwa mshika kibendera huku mwenzake Mussa Hassan Mgosi akitolewa baada ya kuchanika kichwa pamoja na mlinda mlango wa Yanga Yaw Berko.


Magoli ya Yanga yalifungwa na Jery Tegete na Shamte Ally aliyefunga katika kipindi cha pili cha dakika za nyongeza huku la Simba likifungwa kwa kwa tuta na Hilary Echesa

Kiimbo cha Malkia kuwasili nchini wiki ijayo

Kifimbo cha malkia wa Elizabeth wa Uingereza kinatarajia kuwasili nchini tarehe ishirini na nane na shamrashamra zake kufanyika tarehe ishirini na tisa kuanzia uwanja wa Uhuru mpaka Ikulu ambapo kitapokewa na Rais Jakaya Kikwete.

Kuwasili kwa kifimbo hicho nchini kunadhihirisha kuanza kwa shamra shamra za michezo ya jumuiya ya madola inayotarajia kuanza kutimua vumbi mwakani katika jiji la New Delhi nchini Tanzania.

Michuano ya Jumuiya ya Madola hushirikisha mataifa yaliywahi kutawaliwa na Uingereza katika kipindi cha ukoloni pamoja na mataifa mengine yaliyoomba uwanachama katika jumuiya hiyo ya madola.

Tuesday, December 22, 2009

Mancini ammezea mate Cassano




Kocha mpya wa klabu ya Manchester City ya Uingereza Roberto Mancini anatarajia kumsajili mshambuliaji wa Sampdoria,Antonio cassano kwa ajili ya kuijaza nafasi ya Craig Bellamy wakati wa usajili wa dirisha dogo la usajili hapo Januari mwakani.

Kwa mujibu wa gazeti la The Daily Mail limeripoti kwamba Mancini anafanya kila jitihada za kumnasa Cassano kwa mara nyingine baada kushindwa kumsajili wakati alipokuwa anaifundisha Inter Milan ya Italia.

Habari kutoka kwa watu wa karibu wa Kocha Mancini zinadokeza kwamba azma hiyo ya kumsajili CASSANO inatokana na ukweli kwamba mshambuliaji Craig Bellamy hana mpango wa kuendelea kukipiga katika klabu hiyo yenye maskani yake jijini Manchester.

Wakati hayo yakiendelea mshambuliaji Roque Santa Cruz wa klabu hiyo amesema hajafurahishwa na kitendo cha kumtimua kocha Mark Hughes kwani mchango wake badon ulikuwa unahitajika hasa katika kipindi hiki,hali hiyo pia imewakumba wachezaji Shay Given,Craig Bellamy ambao pia hawajafurhishwa na kuondoka kwa kocha Mark Hughes.

Friday, December 18, 2009

UEFA YAMREJESHA MAURINHO STAMFORD BRIDGE


Shrikisho la mpira wa miguu barani ulaya UEFA limetangaza mechi za hatua ya mtoano za ligi ya mabingwa barani ulaya ambapo kocha wa zamani wa klabu ya Chelsea abaye kwa sasa anainoa klabu ya Inter Milan Jose Maurinho atakutana uso kwa uso na klabu yake hiyo ya zamani katika hatua ya makundi.


Wakati Inter Milan ikikutana na Chelsea, Manchester United itacheza na Ac Milan katika hatua hiyo na mchezo huo unaweza ukamrudisha David Beckham katika dimba la Old Trafford akiwa anacheza dhidi ya timu yake hiyo ya zamani.


Michezo mingine inayotarajia kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka ni kama ifuatao


Stuttgart v Barcelona

Olympiakos v Bordeaux

Inter Milan v Chelsea

Bayern Munich v Fiorentina

CSKA Moscow v Sevilla

Lyon v Real Madrid

Porto v Arsenal

YANGA YAFANYA MAUAJI KWA MAFUNZO


Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara imeshusha kipigo kitakatifu kwa mabingwa wa Zanzibar klabu ya Mafunzo mara baada ya kuicharaza goli sita kwa buyu katika mchezo wa kombe la Tusker na kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.


Alikuwa ni Jery Tegete ndiye aliyekwamisha magoli matatu pekee huku mfungaji bora wa michuano ya Challenge Mrisho Khalfan Ngasa akikwamisha magoli mawili na mkenya Boniface Ambani akipigilia msumali wa mwisho kwa kupachika goli la sita.


Yanga sasa itaikabili Tusker ya Kenya katika mchezo wake wa mwisho wa hatua ya makundi junmapili ya wiki hii ambapo mchezo huo ndio utakaotoa picha ni timu zipi zitakutana katika hatua ya nusu fainali ya kombe hilo japo hali inavyoonesha, Simba na Yanga ambao ni wapinzani wa jadi wananafasi kubwa sana ya kukutana katika hatua hiyo.



OMONDI: SIJAJA TANZANIA KUTALIII! BALI KUSHINDA


Bondia kutoka nchini Uganda ambaye anafanya kazi zake nchini Japan, Festus Omondi amesema hajaja nchini kutalii bali amekuja kushinda na kuchukua mkanda wa UBO unaoshikiliwa kwa sasa na bondia mahiri hapa nchini Mbwana Mtumla.


Omondi ambaye anaonekana kujiamini sana, amesema licha ya mashabiki wengi wa hapa nchini kumuona kama mchovu lakini anachoweza kuwaambia sasa hivi yupo tayari kumvaa Mbwana Matumla ambaye kwa upande wake amesema hawezi kutoa tambo kabla mechi lakini ataonesha makeke yake ndani ya ulingo hapo kesho.


Licha ya kuwania mkanda huo, pia mabondia hao watawania mkanda ulio wazi unaotambulia na shirikisho la ngumi za dunia ICB ambao umetolewa na shirikisho hilo kwa ajili ya kuhamasisha mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini.

CHEKA AAHIDI KICHEKO KWA WATANZANIA HAPO KESHO


Bingwa wa dunia anayeshikilia mkanda wa ICB, Francis Cheka ametamba kumtwangwa mpinzani wake Erique Areco kutoka Argentina hapo kesho katika pambano la kuwania ubingwa wa dunia wa mkanda wa mkanda wa ICB uzito wa kati.


Akiongea na blog hii ya spotidesk, bondiia huyo ambaye maskani yake yapo Morogoro amesema hakuna kitakachoweza kumzuia hapo kesho yeye kushindwa kumchapa Areco kutokana na kufanya mazoezi makali pamoja na sapoti atakayoipata kutoka kwa watanzania ambao watakuwa wakmshabikia.


Chekaanatarajia kupanda ulingoni hapo kesho kucheza na Areco katika pambano la round kumi a mbili litakalofanyika katika ukumbi wa PTA uliopo Temeke jijini Dar es Salaam.

Thursday, December 17, 2009

Uhuru kitendawili kuikabili Mtibwa kesho


Mshambuliaji machachari wa klabu ya Simba Uhuru Selemani yupo mashakani kuikabili Mtibwa hapo kesho katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Tusker.


Uhuru yupo kutokana na kukabiliwa na tatizo la misuli ambalo allipata katika mchezo dhidi ya sofapakaka uliochezwa alhamisi ya wiki hii hali iliyomfanya ashindwe kurudi tena uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Kijuso.


Endapo Uhuru ataukosa mchezo huo, hilo litakuwa pigo kubwa kwa kocha mkuu wa klabu hiyo Patrick Phiri ambaye tayari anamkosa mshambuliaji wake machachari na mwenye kasi Danny Mrwanda anayekabiliwa na tatizo la misuli.


Katika mchezo dhidi ya Mtibwa, Simba itahitaji ushindi wowote ama sare ili iweze kufuzu kucheza hatua ya nusu fainali ya kombe hilo linaloshirikisha mataifa kutoka ukanda wa Afrika Mshariki.

SIMBA, SOFAPAKA HAKUNA MBABE


Klabu ya soka ya Simba imeanza michuano ya kombe la Tusker kwa sare ya bila kufungana na mabingwa wa Kenya Sofapaka katika dimba la uhuru jioni ya leo. Sofapaka ambao waliirarua Mtibwa bao tatu bila hapo jumanne, walielemewa kwa muda mwingi wa mchezo lakini washambuliaji wa wekundu wa msimbazi hawakuwa makini kutumia nafasi lukuki walizopata.

katika kipindi cha kwanza Mussa Hassan Mgosi alikosa penalti baada ya Hilarry Echesa kuchezewa vibaya katika eneo la hatari.


Mara baada ya mwamuzi kupuliza kipenga cha mwisho, kocha mkuu wa klabu ya simba, Patrick Phiri amesema timu yake imeonesha kandanda safi sema safu yake ya ushambuliaji imeshindwa kumalizia nafasi ambazo ilizipata na amewaahidi mashabiki wa klabu hiyo kuwa klabu yake itaondoka na ushindi katika mchezo wake wa mwisho katika hatua ya makundi dhidi ya Mtibwa.


Wakati Phiri akisema hayo, kocha mkuu wa Sofapaka na mshambuliaji mahiri wa klabu hiyo Patrick Kagongo wamemlalamikia mwamuzi kwa kipendelea Simba na wamesema kuwa Simba ni klabu kubwa hivyo inapaswa kuacha kucheza na waamuzi.


Michuano hiyo inayochezwa katika dimba la uhuru inatarajia kuendelea ijumaa ya wiki hii kwa mabingwa wa soka nchini Yanga kuteremka dimbani kucheza na Mafunzo kutoka Zanzibar mchezo ambao unatarajiwa kuwa wa vuta ni kuvute kwakuwa Mafunzo itahitaji kushinda ili iingie katika hatua ya nusu fainali.