RT
Chama cha riadha nchini kimesema hakihusiki na utoaji wa ruhusa wa matumizi ya uwanja wa taifa kwa wachezaji wa timu ya taifa ya riadha inayofanya mazoezi katika uwanja wa uhuru kujiandaa na michezo ya jumuiya ya madola yatakayofanyika hapo baadae katika jiji la New Delhi nchini India.
Akiongea na redio Mlimani, katibu mkuu wa RT, Selemani Nyambui amesema, wizara ya habari, utamaduni na michezo ndiyo inadhamana ya kutoa ruhusu kwa timu hiyo kufanyia mazoezi yao katika uwanja huo wenye sifa na viwango vyote vya olimpic.
Hapo awali, dawati la michezo la redio mlimani lilitembelea katika kambi ya timu ya taifa ya riadha na kuonana na kocha wake mkuu Adrew Baro ambaye alieleza bayana kuwa timu yake inakabiliwa na mazingira magumu yakufanyia mazoezi katika uwanja wa uhuru kwakua uwanja huo hauna sifa zozote za mchezo wa riadha.
Kocha huyo raia wa Cuba ameongeza na kusema kuwa, wameshapeleka barua wizarani ya kuomba kupaiwa uwanja huo japo mara mbili kwa wiki lakini hadi sasa jitihada zao zimegonga mwamba na hawaelewi nini tatizo.
Mwishoni mwa mwaka jana wakati wa hafla ya kupokea kifimbo cha malkia cha michezo ya jumuiya ya madola, Rais Jakaya Kikwete ambae ni mdau mkubwa wa michezo aliweka bayana kuwa dhamira ya serikali yake kwa sasa ni kuuinua mchezo wa riadha ambao katika miaka ya hivi karibuni umedorora tofauti na miaka ya nyuma.